Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

Wakala ya mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA) yaendesha mafunzo ya siku tano ya huduma bora kwa wateja mjini Morogoro. Mafunzo hayo yanashirikisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali, baada ya kozi hiyo washiriki watakabidhiwa vyeti vya ushiriki.

Mkufunzi mkuu wa kozi hiyo Dkt. Yustin Bangi alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwafundisha washiriki jinsi ya kuwahudumia wateja wakorofi, kujiamini kwenye maongezi ya simu, jinsi ya kuvutia wateja wapya na kuwaridhisha wateja waliopo ili waendelee kutumia huduma za taasisi husika. Vilevile kuwawezesha na kuwajengea washiriki uwezo zaidi wa kiutendaji na kuwaongeza ufanisi katika kuhudumia wateja kwa kutoa huduma bora ili kutimiza malengo na majukumu yao na vile vile kuendana na kasi ya sasa ya ukuaji wa uchumi na mapinduzi ya viwanda.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.

TaGLA ni mwanachama wa Mtandao wa Vituo vya Mafunzo ya Maendeleo barani Afrika (AADLC). AADLC ina jukumu la kuwawezesha watoa maamuzi na wataalamu pamoja na watendaji kupata na kushirikishana uzoefu na ujuzi uliopo duniani  kupitia mifumo ya mawasiliano kwa njia ya mtandao.

Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) inaiwakilisha Tanzania kwenye kongamano la kimataifa la Elimu Masafa barani Afrika  linalofanyika jijini Kigali nchini Rwanda.

Akifungua kongamano hilo mwenyekiti wa AADLC Ndg. Aliuo Mohamedi kutoka Mali alisema kongamano hilo linashirikisha vituo vya  Mtandao wa Mafunzo ya Maendeleo barani Afrika kutoka nchi mbalimbali.  Pamoja na ajenda kuu ya elimu masafa washiriki  pia walijadiliana masuala mbalimbali ya mtandao wao kwa lengo la kuuboresha mtandao huo ili ulete mageuzi na mapinduzi ya mawasiliano ya kiteknolojia barani Afrika, vile vile washiriki walibadilishana uzoefu, kwa mfano Dkt. Nfuka alifafanua jinsi TEHAMA  inavyotumika kama nyenzo wezeshi kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa Mfumo wa Ujifunzaji Kielektroniki (MUKI) kwenye  kutoa  mafunzo ya madiwani kwa njia ya elimu masafa nchini Tanzania ukizingatia vifaa walivyonavyo madiwani kwa kutumia simu zao za kiganjani kufanya  kila kitu: kusoma, kuangalia video, kutafakari, kufanya mazoezi, majadiliano, soga, kufanya mitihani na tathmini.

Nchi zinazoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Benin, Mali, Uganda, Kenya, Tanzania na Ivory Coast.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.

Wakala ya mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA) yaendesha mafunzo ya siku tano kwa watumishi mbalimbali walio katika ajira rasmi  mjini Mrogoro. Warsha hiyo ya siku tano imeshirikisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali nchini, baada ya warsha hiyo washiriki walikabidhiwa vyeti vya ushiriki.

Akitoa mafunzo hayo, mkufunzi Nd. Anselm Namala alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa washiriki maarifa, mbinu na uzoefu wa jinsi ya kujiandaa vema na maisha baada ya kustaafu, kwani tafiti mbalimbali zimebaini kuwa wastaafu wengi hukumbwa na misukosuko mingi ya kifedha, kiafya na kimaisha kwa ujumla. Moja kati ya sababu kubwa ya wastaafu kukumbwa na misukosuko hiyo na kushindwa kuihimili vema ni kutokuwa na mipango madhubuti ya maisha baada ya kustaafu kazi.

Mafunzo ya Kujiandaa na Maisha Baada ya Kustaafu Kazi yamelenga kumwezesha mfanyakazi kuanza kujiandaa kisaikolojia juu ya maisha baada ya kustaafu, kuwaelimisha juu ya kuandaa mpango binafsi wa kustaafu, kuwapa mbinu za kijasiriamali na stadi za maisha na kutoa elimu ya afya. Mafunzo hayo pia yalitoa fursa kwa washiriki kubadilishana ufahamu na uzoefu kutokana na mazingira watokayo lakini pia walipata fursa ya kutembelea miradi ya ufugaji wa kuku na samaki.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.

Matumizi jumuishi ya TEHAMA huleta ufanisi katika kufikia malengo na kuweka mifumo ya majiji endelevu duniani, ikiwemo Tanzania. Hii ilibainika kupitia mada iliyowasilishwa na Dkt. Hee-Su Kim kutoka Chuo cha Maendelo cha Korea jijini Seoul, Korea ya Kusini kupitia mtandao wa videoconference, akitoa uzoefu wa nchini Korea Kusini juu ya jukwaa jipya na mapinduzi ya nne ya viwanda katika  kuleta maendeleo endelevu ya majiji  nchini Korea Kusini. Pamoja na mambo mengine , washiriki walibadilishana uzoefu na kuuliza maswali kuhusu mikakati ya kukuza majiji na kuleta mapinduzi ya viwanda ili  kufikia maendeleo endelevu katika majiji.

Baada ya semina hiyo washiriki wa Tanzania wakiongozwa na mkurugenzi mtendaji wa TaGLA, Nd. Charles Senkondo walibadilishana uzoefu  kwa kuchangia mawazo na hatua zipi zichukuliwe ili kutatua changamoto za miji na majiji yetu kwa kuiga mfano wa Korea Kusini ili isaidie ukuaji wa majiji yetu na kuleta mapinduzi ya viwanda. Washiriki waliona ipo haja ya kuandaa jukwaa la kitaifa na kuwashirikisha wadau kutoka sekta muhimu nchini ili kujadili suala la ukuaji wa miji na mapinduzi ya viwanda.

Semina hii ni muendelezo wa semina za Majji Endelevu, na  zitakuwepo kwa vipindi mfululizo mwaka huu.

Nchi zinazoshiriki katika semina hii ni pamoja na China, Vietnam, Philippines, Indonesia, Thailand, Bangladesh, Nepal, Sri Lanka, India, Tanzania na Korea Kusini.

Wito unatolewa kwa watanzania kutumia fursa hii ili kupata fursa ya kubadilishana mawazo na kubuni mbinu mpya za kuiwezesha Tanzania kuwa na majiji endelevu ya mfano kuweza kuiweka katika utayari wa kuwa nchi ya viwanda.

TaGLA imeendelea kuiwakilisha vyema Tanzania na bara la Afrika katika kushiriki Semina za Majiji Endelevu zilizoandaliwa kwa kushirikiana na Chuo cha Maendeleo nchini Korea Kusini kwa Njia ya Mtandao wa Mawasiliano ya Video (Video Conference).

Mada iliyowasilishwa na Jin Hwa Kim kutoka Chuo cha Maendelo cha Korea jijini Seoul, Korea ya Kusini ilitoa uzoefu wa kutoka nchini Korea Kusini katika kukuza majiji ya kiutawala ili kuleta maendeleo  kutokana na uzoefu wa Korea Kusini kuanzisha jiji la kiutawala la Sejong. Katika mjadala huu, maandalizi mahsusi yalifanyika kuhakikisha mazingira bora ya kuishi na kufanya kazi yanaendelezwa, huduma za kijamii zinaandaliwa na kutolewa katika kanda maalum za jiji na hatua maalum zinachukuliwa ili taasisi za elimu zianzishe matawi ya kuhudumia watumishi na familia zao.

Washiriki wa Tanzania kutoka Halmashauri za Majiji, sekta binafsi, mifuko ya hifadhi ya jamii na taasisi za elimu walishiriki kwa kuchangia uzoefu katika kutatua changamoto za majiji ya nchi zinazoendelea na kupata mrejesho kutoka Korea na nchi nyingine.

Semina hii ni muendelezo wa semina za Miji Endelevu, na  zitakuwepo kwa vipindi vingine vitatu kati ya sasa na Oktoba 2018, ikijumuisha tarehe 11 Septemba, tarehe 18 Septemba na tarehe 11 Oktoba 2018.

 Nchi zinazoshiriki katika semina hii ni pamoja na China, Vietnam, Philippines, Indonesia, Thailand, Bangladesh, Nepal, Sri Lanka, India, Tanzania na Korea Kusini. Washirki kutoka nchi hizo walipata wasaa wa kuuliza maswali na maswali yao yalijibiwa mubashara na mtoa mada kutoka  Korea Kusini kupitia njia ya mtandao wa mawasiliano ya video.

TaGLA  imekuwa kiungo muhimu katika jukwaa la mafunzo ya leseni ya kimataifa ya utumiaji kompyuta lililoshirikisha vituo tisa vya Tanzania ( Accredited Testing Centers)). Hii ilidhihirika wakati wa jukwaa hilo lililofanyika  kwa ufanisi mkubwa katika ofisi za Wakala zilizopo jijini Dar es Salaam.

Akiwakaribisha washiriki wa jukwaa hilo kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa TaGLA, Meneja wa Habari na Mafunzo Ndg. Dickson Mwanyika aliishukuru ICDL Afrika kwa kushirikiana na TaGLA katika kuandaa jukwaa hilo kwa kuwa litasaidia sana kuondoa changamoto , kutumia fursa zilizopo katika kupata ufumbuzi katika mafunzo ya kiteknolojia  na kuwataka washiriki wengine kutoka vituo vingine kushirikiana vyema ili kutatua changamoto zinazokabili  nchi yetu katika masuala ya matumizi ya teknolojia kurahisisha utoaji huduma.

Katika jukwaa hilo, mambo muhimu yalijadiliwa ni pamoja na  kuboresha huduma zitolewazo kwa kutumia TEHAMA, kujenga uwezo wa wanachama na kuongeza idadi ya wanachama barani Afrika.

TaGLA ni mojawapo kati ya vituo 9 vya Tanzania vilivyosajiliwa na  ICDL Afrika katika kutoa mafunzo na kufanyia mitihani ya leseni ya kimataifa ya utumiaji kompyuta.

Umuhimu wa uwiano wa makazi bora, elimu na miundombinu bora katika majiji wabainika katika semina ya Majiji Endelevu duniani huko Korea Kusini kupitia Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao Tanzania (TaGLA)

TaGLA imeendelea kuiwakilisha vyema Tanzania na bara la Afrika katika kushiriki Semina za Majiji Endelevu zilizoandaliwa kwa kushirikiana na Chuo cha Maendeleo nchini Korea Kusini kwa Njia Ya Mtandao wa Mawasiliano ya Video (Video Conference).

Akitoa taarifa fupi na kuwakaribisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali kwenye semina hiyo iliyofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Nd. Charles Senkondo alieleza kuwa washiriki kutoka taasisi mbalimbali Tanzania watajumuika pamoja na washiriki  zaidi ya 160 kutoka nchi 11 duniani kubadilishana uzoefu kuhusu Majiji Endelevu.

 Mada iliyowasilishwa na Prof. Jeong – Ho Kim kutoka Chuo cha Maendelo cha Korea jijini Seoul, Korea ya Kusini ilitoa uzoefu wa kutoka nchini Korea Kusini katika kukuza majiji yao kimkakati ili kuweza kuvutia wawekezaji na kuleta maendeleo endelevu ya majiji hususan mpango mkakati wa maboresho ya serikali za mitaa, somo kutokana na sera na uzoefu wa jiji la Seoul. Katika mjadala huu, umuhimu wa uwiano wa makazi bora, elimu na miundombinu bora katika majiji vilibainika katika semina hii ya Majiji Endelevu duniani huko Korea Kusini. Maeneo mengine yaliyobainika ni pamoja na uwiano wa huduma za kijamii na uwezo wa eneo kujitegemea kifedha.

Washiriki wa Tanzania kutoka Halmashauri za Majiji, sekta binafsi, mifuko ya hifadhi ya jamii na taasisi za elimu walishiriki kwa kuchangia uzoefu katika kutatua changamoto za majiji ya nchi zinazoendelea na kupata mrejesho kutoka Korea na nchi nyingine.

Semina hii ni muendelezo wa semina za Miji Endelevu, na  zitakuwepo kwa vipindi vingine vinne kati ya sasa na Oktoba 2018, ikijumuisha tarehe 26 Julai, tarehe 11 Septemba, tarehe 18 Septemba na tarehe 11 Oktoba 2018.

 Nchi zinazoshiriki katika semina hii ni pamoja na China, Vietnam, Philippines, Indonesia, Thailand, Bangladesh, Nepal, Sri Lanka, India, Tanzania na Korea Kusini.

TaGLA ni wakala ya Serikali ya mafunzo kwa njia ya mtandao. Ni moja wapo kati ya mtandao wa vituo zaidi ya 120 duniani (www.gdln.org)

Wito unatolewa kwa watanzania kutumia fursa hii ili kupata fursa ya kubadilishana mawazo na kubuni mbinu mpya za kuweza kuiweka Tanzania katika utayari wa kuwa nchi ya viwanda.

Tanzania imekuwa kiungo muhimu katika utoaji huduma za mikutano na mafunzo kwa njia ya Video (Videoconference) kupitia huduma pekee za Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA). Hii ilidhihirika wakati wa Kikao cha Kazi kilichofanyika kwa ufanisi kupitia huduma ya Daraja Video itolewayo na TaGLA kwa kuunganisha wanachama wa Mtandao wa Vituo vya Maendeleo barani Afrika (AADLC, www.aadlc.net) uliojumuisha nchi za Benin, Cote d’ Ivore, Kenya, Mali, Senegal, Tanzania na Uganda.

Akiongoza Mkutano huo Mwenyekiti wake Ndg. Aliuo Mohamed kutoka Mali aliishukuru TaGLA kwa kuwa kiungo muhimu katika mtandao kwa kutoa huduma bora ya Daraja Video (Videoconference bridging) na kuwataka wanachama wengine kushirikiana vyema ili kutoa nyenzo ya ufanisi na kutatua changamoto zinazokabili  bara la Afrika.

Katika kikao hicho, mambo muhimu yalijadiliwa ikiwemo kuboresha huduma zitolewazo ikiwemo TEHAMA, kujenga uwezo wa wanachama na mbinu za kuongeza idadi ya wanachama barani Afrika.

TaGLA ni mwanachama wa AADLC na pia ni mwanachama wa GDLN (Global Development Learning Network) yenye vituo vya maendeleo zaidi ya 120 duniani.

Tafadhali tembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na Wakala.