Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

Balozi Ombeni Sefue afanya kweli katika matumizi ya TEHAMA, TaGLA

Balozi Ombeni Sefue, Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Watoa Huduma za Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS) aonyesha njia rahisi ya kuokoa muda,  adha ya safari na gharama kwa kutoa mada juu ya Utawala wa Mafuta na Gesi kwa kutumia teknolojia ya videoconference wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao, TaGLA.

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na TaGLA yamejumusiha washiriki kutoka taasisi mbalimbali zinazohusika katika masuala ya mafuta na gesi katika kumbi za Wakala hiyo jijini Arusha.

Akiwasilisha mada kwa njia ya Mtandao, Balozi Sefue amesisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo watendaji na Watanzania kwa ujumla ili kuweza kushiriki kukamilifu katika fursa zinazoletwa na uvumbuzi wa mafuta na gesi.

Balozi sefue ameshukuru TaGLA kwa huduma bora za mtandao wa videoconference unaowezesha kuongeza ufanisi na kuondoa adha za kusafiri. Alisema kuwa, kwa kutumia huduma hii, aliweza kuongea na kuwasilisha mada akiwa TaGLA Dar es Salaam  kwa ufanisi , na kuwa na nafasi ya kujadiliana na washiriki walioko Arusha.

Balozi Sefue alisisitiza kuwa katika suala zima la Usimamizi na Utawala Bora wa rasilimali zetu hasa “Mafuta na Gesi” inabidi kushirikisha wadau wote na wananchi kwa ujumla namna ya kutumia rasilimali hii baada ya kuipata ili isaidie nchi kwa miaka kwa faida ya vizazi vijavyo ijayo hata rasilimali zinakapokuwa zimeisha. Alisisitiza jambo moja kuwa Watanzania tunahitaji kujifunza kwa upande wa rasilimali zetu, usemi unaosema “Usinisaidie kufanya yote bali niachie nifanye mwenyewe” kwa lugha ya kigeni “Don’t do it for me, Give me capacity to do it myself”.

Kwa upande wa washiriki walioko Arusha, walifurahi sana kupata uwasilisho kutoka kwa Balozi  kuwa umejikita katika maeneo muhimu ambayo ndiyo changamoto katika nchi yetu hasa tunavyojiandaa na ugunduzi wa mafuta na gesi asilia. Jambo moja la kuangalia ni fursa zipi ambazo Watanzania wajiandae kuzichukua na muhimu zaidi kujua mapema ni maeneo gani ambayo huduma gani zitakazohitajika wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa hasa.

Kwa upande wake , Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA  Bw. Charles Senkondo, ametoa wito wa watanzania kuendelea kutumia huduma za Wakala hiyo ili kuendana na kasi ya maendeleo inayohitajika kwa kuokoa muda na gharama zinazoweza kuepukika kwa kutumia huduma za wakala. Wakala ya Mafunzo kwa njia ya Mtandao ilianzishwa mwaka 2011 chini ya Ofisi ya Rais Utumushi ikiwa na majukumu ya kutoa nafasi pekee ya kimataifa kwa ajili ya mafunzo ya maendeleo kwa Watanzania na kuwezesha ukuaji wa taaluma mbalimbali kupitia mitandao ya maendeleo duniani.