Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

TAGLA YAWEZESHA MAFUNZO KWA WATENDAJI WAKUU WA MASHIRIKA YA UMMA, WENYEVITI NA WAJUMBE WA BODI KUHUSU UWAJIBIKAJI NA UTENDAJI

Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) waliandaa mafunzo kwa Watendaji wakuu, Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma. Mafunzo hayo yalijikita katika maeneo ya kukumbushana Majukumu yao katika utendaji kazi wa kila siku uwajibikaji na utawala bora, katika Mafunzo hayo Mgeni rasmi alikuwa Naibu Katibu Mkuu Bibi. Amina Kh. Shaabani.  

Mheshimiwa Bi. Amina alisema mtakumbuka kuwa, kuanzia miaka ya 1990, Serikali iliamua kurekebisha Mashirika ya Umma kwa lengo la kuyapa ufanisi ili yaendane na kasi ya mabadiliko makubwa ya kiuchumi yanayoendelea duniani katika mifumo ya uchumi, biashara, jamii, na hata uendeshwaji wa shughuli za Serikali ambapo mabadiliko haya yamesababisha Serikali yetu iendelee kuboresha uendeshaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma. Katika kutekeleza lengo hili, tulivunja SCOPO mwaka 1992 na kuhamishia majukumu yake mengi Ofisi ya Msajili wa Hazina na tukatunga Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992 na marekebisho yake ya mwaka 1993 na 2010 ili kuboresha usimamizi na kuleta tija katika Taasisi na Mashirika ya Umma.

Mgeni rasmi Bi Amina alisema kuwa, mwezi Mei 2010, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilirekebisha Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya mwaka 2002 na kuifanya Ofisi inayojitegemea ili kuboresha uendeshaji na usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma katika dhana nzima ya kuruhusu ushindani katika soko la Uchumi huria. Tumelazimika leo kuwa na mafunzo haya ili kukumbushana Majukumu ya Watendaji wa Mashirika na Taasisi za Umma Pamoja na Bodi za Wakurugenzi. Aliendelea kuwa, kama mnavyofahamu, kufuatana na Sheria mbalimbali zinazounda Mashirika ya Umma, kila Shirika lina Mtendaji Mkuu pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ambayo ina wajibu wa kuiongoza Menejimenti katika utekelezaji wa .......

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania akichangia mada wakati wa Mafunzo ya Uwajibikaji kwa Watendaji Wakuu na Wajumbe wa Bodi Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania akichangia mada wakati wa Mafunzo ya Uwajibikaji kwa Watendaji Wakuu na Wajumbe wa Bodi

majukumu ya Shirika husika.

Alisisitiza kuwa, kufanikiwa  kwa  Mashirika  ya  Umma  kunategemea  sana  uimara  wa  Bodi za Wakurugenzi ambazo zinazingatia majukumu na mipaka yake ya kazi.  Bodi ya Wakurugenzi   inawajibika kufuatilia, kusaidia na kuiwezesha Menejimenti ya Mashirika/Taasisi za Umma kuinua tija na kuongeza ufanisi alimaliza.

Naye Kaimu Msajili wa Hazina Dkt. Maftah Bunini katika hotuba yake ya ufunguzi alisisitiza kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa mamlaka ya kisheria ya kusimamia Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma kupitia Vifungu Na. 10 (2) (e) na 10 (5) vya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 (kama ilivyorekebishwa mwaka 2010). Kupitia Sheria hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina ina wajibu wa kusimamia utendaji wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu katika Taasisi/Mashirika husika unafanyika kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali. Katika usimamizi huo, Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma ambazo Serikali ni Mwanahisa Mkuu. Aidha, katika Mashirika au Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache, Ofisi ya Msajili wa Hazina huchagua wawakilishi wake katika Bodi za Wakurugenzi.

Alieleza kuwa, Bodi ya Wakurugenzi ndiyo chombo cha juu cha usimamizi wa utendaji wa Taasisi au Shirika. Kulingana na Sheria ya kuanzishwa kwa Taasisi/Shirika, kila Taasisi/Shirika linapaswa kuwa na Bodi ya Wakurugenzi inayosimamia Menejimenti katika utekelezaji wa majukumu yake. Kufanikiwa kwa Taasisi/ Mashirika ya Umma kunategemea sana uimara na weledi wa Bodi za Wakurugenzi katika kusimamia utendaji wa majukumu ya Taasisi/Mashirika husika. Majukumu ya msingi ya Bodi za Wakurugenzi yameainishwa katika Kifungu cha 8 cha Sheria ya Mashirika ya Umma Na.2 ya mwaka 1992.  Ofisi ya Msajili wa Hazina iliandaa vigezo kwa Mamlaka za uteuzi kuhusu sifa na vigezo vya uteuzi wa Wajumbe wa Bodi katika Mashirika na Taasisi za Umma ili kuwa na watu wenye sifa na weledi katika usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma.

Msajili wa hazina aliendelea kusema kuwa, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea kutekeleza jukumu lake la usimamizi wa Bodi kwa kuhakikisha zinakuwa hai na kuwa na Wajumbe wenye weledi wa kutosha. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2017, Taasisi na Mashirika ya Umma yapatayo 181 (77%) kati ya 234 yalikuwa na Bodi zilizo hai. Aidha, Taasisi na Mashirika ya Umma yapatayo 53 hayakuwa na Bodi za Wakurugenzi.

Alisema kuwa, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeandaa nyenzo ya Tathmini ya utendaji kazi wa Bodi (Board Evaluation Tool). Nyenzo hii inatumiwa na Wajumbe wa Bodi kutathmini utendaji wa kila mmoja wao na kufanya tathmini ya Bodi nzima kwa ujumla katika kipindi cha mwaka husika na kipindi chote wanachohudumu katika Bodi hiyo. Nyenzo hii imeisaidia Ofisi ya Msajili wa Hazina kupata tathmini ya utendaji wa Mjumbe mmoja mmoja na kwa Bodi nzima na kuwezesha kutoa ushauri kwa Mamlaka ya uteuzi juu ya utendaji wa Wajumbe wa Bodi.

Msajili wa Hazina wakati akimkaribisha Mtendaji Mkuu wa Wakala ya mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA), ili kuweza kuendelea na ratiba kamili ya mafunzo ambayo yametolewa na Wakala alisisitiza kuwa wakala imepewa mamlaka na serikali kujenga uwezo wa utendaji kazi katika taasisi zetu. Ni Wakala ya Serikali ambayo ipo chini ya Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Hivyo tuitumie katika kuboresha tija katika taasisi zetu na bodi zetu.

Wakati wa kukaribisha watoa mada iliyoratibiwa na Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA), Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala hiyo Ndg. Charles Senkondo alielezea kuwa Wajumbe wengi wamekuwa wakifikiria kuwa Wakala yetu siyo taasisi ya Serikali, na kuongeza kuwa TaGLA ni chombo cha Serikali kilichoanzishwa na Sheria ya Wakala za Serikali kupitia Ofisi ya Raisi Utumishi ikiwa na jukumu la kujenga uwezo wa taasisi za Umma na serikali katika kuongeza ufanisi wa kazi na utendaji wao kwa ujumla. Alieleza kuwa kazi kubwa ni kuhakikisha mafunzo yanaandaliwa kwa ueledi yakizingatia mahitaji sahihi na kwa wakati muafaka. Aliendelea kuwa wakala imeandaa mafunzo mengi ya kuhakikisha Wajumbe wa Bodi na Menejimenti za mashirika mbalimbali wanapata mafunzo stahiki ili kuweza kusimamia taasisi zao vizuri. Katika mafunzo haya ya leo ni kama kuwaonjesha tu ila mafunzo yapo mengi kama vile  mafunzo ya “Kuwasimika wajumbe wa Bodi” (Board Induction), Tathmini ya Utendaji wa Bodi “Board Self Evaluation”, Utawala Bora katika Bodi (Board Governance ), Usimamizi wa Viashiria hatari kusimamia Utendaji wa bodi (Board Risk Management and Risk Oversight) na Namna ya Kujifanyia Tathmini ya utendaji wa Bodi (Board Self-Assessment and Reporting) n.k.

Akiwakaribisha watoa mada, katika maeneo ya Utawala bora, Uwajibikaji na Maadili Mkurugenzi wa Wakala  Ndg Senkondo alieleza kuwa wataalamu ambao wakala imesheheni ni wazoefu wa Utumishi wa Umma ambao wameshafanya kazi kwa miaka mingi na wanao uzoefu kufanya kazi za umma hivyo alisisitiza kuwa taasisi zote za umma zinahitajika kutoa mafunzo muafaka kwa Bodi zao na watendaji wao ili kuweza kwenda na kasi ya Utendaji kazi wa Serikali awamu ya Tano. Mada tatu zilitolewa kama ifuatavyo: -

Mada ya Kwanza: Majukumu ya Bodi za Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (imetolewa na Kaimu Msajili wa Hazina);

Mada ya Pili: Usimamizi na Uwajibikaji wa Bodi za Wakurugenzi katika Taasisi na Mashirika ya Umma iliyotolewa na TaGLA mwezeshaji akiwa Ndg. Yona Killagane.

Mada ya Tatu: Maadili na Wajumbe wa  Bodi za Wakarugenzi na Mashirika ya Umma iliyotolewa na TaGLA mwezeshaji akiwa Ndg. Lodovick Utouh.

Katika majadiliano kuhusu mada wajumbe walifurahi sana kupata mada kutoka kwa watoa mada wazoefu katika Utumishi wa Umma na hasa katika utendaji wao uliotukuka.

Katika kufunga mafunzo hayo Kaimu Msajili wa Hazina alitoa wito kwa Taasisi zote za Serikali kutumia Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao kwani wameonyesha kumudu mahitaji ya Wadau na pia wanauwezo wa kutoa mafunzo kwa Bodi na Menejimenti za Taasisi za Umma zote. TaGLA ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa ikiwa na jukumu la kujenga uwezo wa watumishi wa umma, Taasis zote za Serikali na sekta binafsi kwa kutumia teknolojia.