Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

TaGLA yafunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wa uongozi wanawake jijiniArusha, Tanzania

Wakala wa Mafunzo kwa Njia ya Mtandao Tanzania (TaGLA) imeendelea na program zake za kutoa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo watanzania.

Washiriki wanawake kutoka taasisi mbalimbali za umma na sekta binafsi  wameshiriki katika mafunzo

hayo ya kuwajengea uwezo wa uongozi yaliyotolewa katika ukumbi wa TaGLA jijini Arusha.

Akifunga mafunzo hayo ya siku tano pamoja na kushuhudia zoezi la utoajiwa vyeti  kwa mtandao wa video akiwa katika ofisi za TaGLA Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA, Nd. Charles Senkondo alieleza kuwa mafunzo hayo yalihudhuriwa na washiriki 14  kutoka taasisi 11 za umma na sekta binafsi. Mkurugenzi aliwapongeza washiriki kwa kuhudhuria mafunzo hayo kwani anaamini washiriki wataenda kuleta mabadiliko katika sehemu zao za kazi baada ya kujengewa uwezo kiuongozi. Alisisitisa kuwa mafunzo haya maalumu kwa ajili ya wanawake waliopo katika uongozi na wale wanaoandaliwa kuwa viongozi ni muhimu kwakuwa yanalenga kuwajengea uwezo wa kutatua changamoto pekee zinazowakwaza wanawake katika kujiendeleza kama viongozi.

Bi Shanta Nagendram kutoka Malaysia, akiongoza uendeshaji wa mafunzo hayo amewapongeza washiriki kwa kutumia muda wao wote  kujifunza mambo mbalimbali ya kuwajengea uwezo katika Nyanja za uongozi ikiwemo Kuongoza Kimkakati, Kujiamini, Kuwasilisha Mada, Kuondoa tabia zinazokinzana na Uongozi Bora, Maadili na Kujiongeza Muonekano.

TaGLA ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Sura ya 245 ikiwa na jukumu la kujenga uwezo wa watumishi wa umma na sekta binafsi kwa kutumia teknolojia na njia bunifu. Pia ni mwanachama wa Chama cha Vituo vya Mafunzo ya Maendeleo barani Afrika (AADLC) na Mtandao wa Mafunzo ya Maendeleo Duniani (GDLN) vyenye jukumu la kuwezesha watoa maamuzi na wataalamu pamoja na watendaji kupata na kushirikishana uzoefu na ujuzi uliopo duniani .

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz  ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.