Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

Viongozi wahimizwa kujinoa kiuongozi

Viongozi wamehimizwa kujinoa kwa kupata mafunzo ya uongozi na kubadilishana uzoefu wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa Uongozi na Menejimenti ya Mabadiliko ya Tabia yanayofanyika katika ukumbi wa TaGLA jijini Arusha.

 Akifungua mafunzo hayo ya siku tano kwa  njia ya mtandao wa video akiwa katika ofisi za TaGLA Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA, Nd. Charles Senkondo aliwakaribisha washiriki walioko jijini Arusha. Mkurugenzi Mtendaji aliwashukuru washiriki kwa kuhudhuria mafunzo hayo kwani anaamini washiriki wataleta  mabadiliko katika utendaji wao na katika sehemu zao za kazi baada ya kujengewa uwezo wa Kiuongozi na Menejimenti ya Mabadiliko ya Tabia. Alisisitiza umuhimu wa viongozi kujinoa kiuongozi ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.

 Mkufunzi kiongozi kutoka nchini India, Bw Avinaash Waikar alisema mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kujitambua wenyewe kwanza kama viongozi na kuwaelewa wengine wanaowaongoza  ili kuleta mabadiliko chanya katika kutimiza malengo na majukumu ya yao na yale ya taasisi zao. Alieleza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kujua aina mbalimbali za uongozi na mbinu gani za uongozi wazitumie ili kuwahamasisha wanaowaongoza kubadilika na kuleta mafanikio.

Akiongea kwa niaba ya Washiriki wa mafunzo hayo akiwa Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa TEMDO Mhandisi Kalutu Koshuma alieleza mategemeo yao ya kuzidi kujijengea uwezo wa kiungozi na kuleta ufanisi unaoendana na kasi ya kuwa na uchumi wa viwanda.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz  ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.