Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

TaGLA yaongeza ufahamu wa Mikakati ya Majiji Endelevu duniani

Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) imeendelea kuiwakilisha vema Tanzania na bara la Afrika kushiriki Semina za Miji Endelevu zilizoandaliwa kwa kushirikiana na Chuo cha Maendeleo nchini Korea Kusini kwa Njia Ya Mtandao wa Mawasiliano ya Video (Video Conference).

Akitoa taarifa fupi na kuwakaribisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali kwenye semina hiyo iliyofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Nd. Charles Senkondo alieleza kuwa washiriki kutoka taasisi mbalimbali Tanzania watajumuika pamoja na washiriki  zaidi ya 160 kutoka nchi 11 duniani kubadilishana uzoefu kuhusu Majiji Endelevu.

 Mada iliyowasilishwa na Ndg. Byoung Ki Kim kutoka Chuo cha Maendelo cha Korea jijini Seoul, Korea ya Kusini ilitoa uzoefu wa nchini Korea Kusini katika kukuza majiji yao kimkakati ili kuweza kuvutia wawekezaji na kuleta maendeleo endelevu ya majiji hususan kutambulisha miradi ya jiji endelevu la Busan nchini Korea Kusini. Pamoja na mambo mengine , washiriki walibadilishana uzoefu kuhusu mikakati ya kuepuka majanga , kuwa na usalama kwa wakazi, kuondoa kero za usafiri na mawasiliano na kujumuisha anuai ili  kufikia maendeleo endelevu katika majiji. Ilibainika kuwa matumizi jumuishi ya TEHAMA huleta ufanisi katika kufikia malengo.

Washiriki wa Tanzania kutoka Halmashauri za Majiji, sekta binafsi, mifuko ya hifadhi ya jamii na taasisi za elimu walishiriki kwa kuchangia uzoefu katika kutatua changamoto za majiji ya nchi zinazoendelea na kupata mrejesho kutoka Korea na nchi nyingine.

Semina hii ni muendelezo wa semina za Miji Endelevu, na  zitakuwepo kwa vipindi vingine vitano kati ya sasa na Oktoba 2018, ikijumuisha tarehe 12 Julai, tarehe 26 Julai, tarehe 11 Septemba, tarehe 18 Septemba na tarehe 11 Oktoba 2018.

 Nchi zinazoshiriki katika semina hii ni pamoja na China, Vietnam, Philippines, Indonesia, Thailand, Bangladesh, Nepal, Sri Lanka, India, Tanzania na Korea Kusini.

TaGLA ni wakala ya Serikali ya mafunzo kwa njia ya mtandao. Ni moja wapo kati ya mtandao wa vituo zaidi ya 120 duniani (www.gdln.org)

Wito unatolewa kwa watanzania kutumia fursa hii ili kupata fursa ya kubadilishana mawazo na kubuni mbinu mpya za kuweza kuiweka Tanzania katika utayari wa kuwa nchi ya viwanda.

Imetolewa na:

Mkurugenzi Mtendaji

Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao,
IFM, Block A, Ghorofa ya Chini,
5 Mtaa wa Shaaban Robert,
S.L.P. 2287,
11101 Dar es Salaam, Tanzania

(+255 22) 2123705, 2123709, 223711

Fax: (+255 22) 2123702

      Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.