Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

Semina ya Majiji Endelevu Duniani Huko Korea Kusini Kupitia Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao Tanzania (Tagla)

Umuhimu wa uwiano wa makazi bora, elimu na miundombinu bora katika majiji wabainika katika semina ya Majiji Endelevu duniani huko Korea Kusini kupitia Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao Tanzania (TaGLA)

TaGLA imeendelea kuiwakilisha vyema Tanzania na bara la Afrika katika kushiriki Semina za Majiji Endelevu zilizoandaliwa kwa kushirikiana na Chuo cha Maendeleo nchini Korea Kusini kwa Njia Ya Mtandao wa Mawasiliano ya Video (Video Conference).

Akitoa taarifa fupi na kuwakaribisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali kwenye semina hiyo iliyofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Nd. Charles Senkondo alieleza kuwa washiriki kutoka taasisi mbalimbali Tanzania watajumuika pamoja na washiriki  zaidi ya 160 kutoka nchi 11 duniani kubadilishana uzoefu kuhusu Majiji Endelevu.

 Mada iliyowasilishwa na Prof. Jeong – Ho Kim kutoka Chuo cha Maendelo cha Korea jijini Seoul, Korea ya Kusini ilitoa uzoefu wa kutoka nchini Korea Kusini katika kukuza majiji yao kimkakati ili kuweza kuvutia wawekezaji na kuleta maendeleo endelevu ya majiji hususan mpango mkakati wa maboresho ya serikali za mitaa, somo kutokana na sera na uzoefu wa jiji la Seoul. Katika mjadala huu, umuhimu wa uwiano wa makazi bora, elimu na miundombinu bora katika majiji vilibainika katika semina hii ya Majiji Endelevu duniani huko Korea Kusini. Maeneo mengine yaliyobainika ni pamoja na uwiano wa huduma za kijamii na uwezo wa eneo kujitegemea kifedha.

Washiriki wa Tanzania kutoka Halmashauri za Majiji, sekta binafsi, mifuko ya hifadhi ya jamii na taasisi za elimu walishiriki kwa kuchangia uzoefu katika kutatua changamoto za majiji ya nchi zinazoendelea na kupata mrejesho kutoka Korea na nchi nyingine.

Semina hii ni muendelezo wa semina za Miji Endelevu, na  zitakuwepo kwa vipindi vingine vinne kati ya sasa na Oktoba 2018, ikijumuisha tarehe 26 Julai, tarehe 11 Septemba, tarehe 18 Septemba na tarehe 11 Oktoba 2018.

 Nchi zinazoshiriki katika semina hii ni pamoja na China, Vietnam, Philippines, Indonesia, Thailand, Bangladesh, Nepal, Sri Lanka, India, Tanzania na Korea Kusini.

TaGLA ni wakala ya Serikali ya mafunzo kwa njia ya mtandao. Ni moja wapo kati ya mtandao wa vituo zaidi ya 120 duniani (www.gdln.org)

Wito unatolewa kwa watanzania kutumia fursa hii ili kupata fursa ya kubadilishana mawazo na kubuni mbinu mpya za kuweza kuiweka Tanzania katika utayari wa kuwa nchi ya viwanda.