Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

TaGLA YAZIDI KUNG’ARA KATIKA SEMINA ZA MAJIJI ENDELEVU DUNIANI KWA NJIA YA MTANDAO WA MAWASILIANO YA VIDEO (VIDEO CONFERENCE)

TaGLA imeendelea kuiwakilisha vyema Tanzania na bara la Afrika katika kushiriki Semina za Majiji Endelevu zilizoandaliwa kwa kushirikiana na Chuo cha Maendeleo nchini Korea Kusini kwa Njia ya Mtandao wa Mawasiliano ya Video (Video Conference).

Mada iliyowasilishwa na Jin Hwa Kim kutoka Chuo cha Maendelo cha Korea jijini Seoul, Korea ya Kusini ilitoa uzoefu wa kutoka nchini Korea Kusini katika kukuza majiji ya kiutawala ili kuleta maendeleo  kutokana na uzoefu wa Korea Kusini kuanzisha jiji la kiutawala la Sejong. Katika mjadala huu, maandalizi mahsusi yalifanyika kuhakikisha mazingira bora ya kuishi na kufanya kazi yanaendelezwa, huduma za kijamii zinaandaliwa na kutolewa katika kanda maalum za jiji na hatua maalum zinachukuliwa ili taasisi za elimu zianzishe matawi ya kuhudumia watumishi na familia zao.

Washiriki wa Tanzania kutoka Halmashauri za Majiji, sekta binafsi, mifuko ya hifadhi ya jamii na taasisi za elimu walishiriki kwa kuchangia uzoefu katika kutatua changamoto za majiji ya nchi zinazoendelea na kupata mrejesho kutoka Korea na nchi nyingine.

Semina hii ni muendelezo wa semina za Miji Endelevu, na  zitakuwepo kwa vipindi vingine vitatu kati ya sasa na Oktoba 2018, ikijumuisha tarehe 11 Septemba, tarehe 18 Septemba na tarehe 11 Oktoba 2018.

 Nchi zinazoshiriki katika semina hii ni pamoja na China, Vietnam, Philippines, Indonesia, Thailand, Bangladesh, Nepal, Sri Lanka, India, Tanzania na Korea Kusini. Washirki kutoka nchi hizo walipata wasaa wa kuuliza maswali na maswali yao yalijibiwa mubashara na mtoa mada kutoka  Korea Kusini kupitia njia ya mtandao wa mawasiliano ya video.