Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

TaGLA YAENDESHA MAFUNZO YA MAISHA BAADA YA KUSTAAFU KAZI KWA WATUMISHI KUTOKA TAASISI MBALIMBALI, MJINI MOROGORO

Wakala ya mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA) yaendesha mafunzo ya siku tano kwa watumishi mbalimbali walio katika ajira rasmi  mjini Mrogoro. Warsha hiyo ya siku tano imeshirikisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali nchini, baada ya warsha hiyo washiriki walikabidhiwa vyeti vya ushiriki.

Akitoa mafunzo hayo, mkufunzi Nd. Anselm Namala alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa washiriki maarifa, mbinu na uzoefu wa jinsi ya kujiandaa vema na maisha baada ya kustaafu, kwani tafiti mbalimbali zimebaini kuwa wastaafu wengi hukumbwa na misukosuko mingi ya kifedha, kiafya na kimaisha kwa ujumla. Moja kati ya sababu kubwa ya wastaafu kukumbwa na misukosuko hiyo na kushindwa kuihimili vema ni kutokuwa na mipango madhubuti ya maisha baada ya kustaafu kazi.

Mafunzo ya Kujiandaa na Maisha Baada ya Kustaafu Kazi yamelenga kumwezesha mfanyakazi kuanza kujiandaa kisaikolojia juu ya maisha baada ya kustaafu, kuwaelimisha juu ya kuandaa mpango binafsi wa kustaafu, kuwapa mbinu za kijasiriamali na stadi za maisha na kutoa elimu ya afya. Mafunzo hayo pia yalitoa fursa kwa washiriki kubadilishana ufahamu na uzoefu kutokana na mazingira watokayo lakini pia walipata fursa ya kutembelea miradi ya ufugaji wa kuku na samaki.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.