Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

TAGLA YASHIRIKI KONGAMANO LA KIMATAIFA LA ELIMU MASAFA BARANI AFRIKA (eLA) JIJINI KIGALI, RWANDA

TaGLA ni mwanachama wa Mtandao wa Vituo vya Mafunzo ya Maendeleo barani Afrika (AADLC). AADLC ina jukumu la kuwawezesha watoa maamuzi na wataalamu pamoja na watendaji kupata na kushirikishana uzoefu na ujuzi uliopo duniani  kupitia mifumo ya mawasiliano kwa njia ya mtandao.

Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) inaiwakilisha Tanzania kwenye kongamano la kimataifa la Elimu Masafa barani Afrika  linalofanyika jijini Kigali nchini Rwanda.

Akifungua kongamano hilo mwenyekiti wa AADLC Ndg. Aliuo Mohamedi kutoka Mali alisema kongamano hilo linashirikisha vituo vya  Mtandao wa Mafunzo ya Maendeleo barani Afrika kutoka nchi mbalimbali.  Pamoja na ajenda kuu ya elimu masafa washiriki  pia walijadiliana masuala mbalimbali ya mtandao wao kwa lengo la kuuboresha mtandao huo ili ulete mageuzi na mapinduzi ya mawasiliano ya kiteknolojia barani Afrika, vile vile washiriki walibadilishana uzoefu, kwa mfano Dkt. Nfuka alifafanua jinsi TEHAMA  inavyotumika kama nyenzo wezeshi kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa Mfumo wa Ujifunzaji Kielektroniki (MUKI) kwenye  kutoa  mafunzo ya madiwani kwa njia ya elimu masafa nchini Tanzania ukizingatia vifaa walivyonavyo madiwani kwa kutumia simu zao za kiganjani kufanya  kila kitu: kusoma, kuangalia video, kutafakari, kufanya mazoezi, majadiliano, soga, kufanya mitihani na tathmini.

Nchi zinazoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Benin, Mali, Uganda, Kenya, Tanzania na Ivory Coast.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.