Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

Ujumbe Kutoka Kenya Watembelea TaGLA

Ujumbe kutoka chuo cha Serikali Kenya (Kenya School of Government - KSG) wametembelea Wakala ya Mafunzo kwa njia ya Mtandao (TaGLA) kwa nia ya kujifunza na kubadilishana uzoefu na Wakala katika maeneo ya elimu/ mafunzo kwa njia ya mtandao na teknolojia ya mikutano kwa njia ya video.

Ujumbe huo kutoka Kenya unaongozwa na Mkuu wa Chuo hicho Dk. Ludeki Chweya,akiongozana na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao na Maendeleo (eLearning and Development Institute) ya nchini Kenya, Ndg. Joseph Ndungu, iliyoko chini ya mwamvuli wa KSG.

Katika ziara yao ya siku mbili (2 - 3 Februari 2017) hapa nchini, ujumbe huu ulipata nafasi ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wakala, lakini pia walipata nafasi ya kutembelea na kufanya mazungumzo na uongozi Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC). Wakuu wa taasisi zote wameona na kusisitiza umuhimu kuboresha mahusiano yaliyopo baina ya taasisi zao lakini pia kuanzisha maeneo mengine ya kushirikiana kwa manufaa ya taasisi zao na nchi zao kwa ujumla.